Karibu katika blog yetu

Wednesday, January 30, 2013

WAHISANI WAKUSANYA PESA ZA KUISAIDIA MALI




Mkutano wa Kimataifa uliowaleta pamoja Viongozi wa nchi za Afrika na Maofisa wa Kimataifa umefanikiwa kukusanya jumla ya dola milioni 600 kwa ajili kusaidia vita vinavyoendelea Kaskazini mwa Mali. Wafadhili mbalimbali wamechangia fedha kwa ajili ya kuendeleza vita iliyopewa jina Vita ya Kupambana na Ugaidi Kaskazini mwa Mali lengo likiwa ni kuyasambaratisha Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanatawala kwa miezi zaidi ya tisa.

Mkutano huo umefanyika nchini Ethiopia ambapo mataifa hayo yameahidi pia kuchangia kijeshi ili kufanikisha kukabiliana na vitendo vya kigaidi ambavyo vyanzo vyake vimekuwa vikitanjwa kuwa nchini Mali.

Japan imechangia dola milioni 120 huku Marekani ikitoa kitita cha dola milioni 96 kati ya dola milioni 600 ambazo zimeahidiwa kutoka kwa nchi ambazo zimehudhuria mkutano huo maalum wa kuchangisha fedha.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa UN, Umoja wa Ulaya EU na China ambao wote wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia operesheni hiyo ya kijeshi.

Rais wa Mali Dioncounda Traore ameishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa mchango ambao wameutoa kwa nchi hiyo katika na kuahidi watakuwa tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali.

Umoja wa Afrika AU umeahidi kutoa dola milioni 50 kusaidia operesheni hiyo ya kijeshi huko Kaskazini mwa Mali ambayo imekadiriwa kugharimu dola milioni 460 ili iweze kukamilika.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AU Nkosazana Dlamini-Zuma amesema wanafahamu kitovu cha mgogoro kwa hiyo ushirikiano ambao wanaupata kutoka Jumuiya ya Kimataifa utasaidia kupata jibu.
Mkutano huo wa kuchangisha fedha kusaidia vita nchini Mali umekuja kipindi hiki ambacho majeshi ya Ufaransa na Mali yakifanikiwa kuweka kwenye himaya yao Mji wa Timbuktu.

No comments:

Post a Comment