Karibu katika blog yetu

Friday, April 19, 2013

KUTOKA TFF


MECHI YA MGAMBO, YANGA YAINGIZA MIL 24/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mgambo Shooting na Yanga iliyochezwa jana (Aprili 17 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga imeingiza sh. 24,865,000 kutokana na watazamaji 4,386.

Viingilio katika mechi hiyo namba 162 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 vilikuwa sh. 10,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 5,547,337.50 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,792,966.10.

Asilimia 15 ya uwanja sh. 2,820,680.08, msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 90,000, waamuzi sh. 270,000, maandalizi ya uwanja sh. 100,000 na tiketi sh. 1,587,500.

Mgawo mwingine ni gharama za mechi sh. 1,692,408.05, Kamati ya Ligi sh. 1,692,408.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 846,204.05 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) sh. 658,158.69.

MAKOCHA AZAM, FAR RABAT KUTETA
Makocha wa timu za Azam, Stewart John Hall na AS FAR Rabat ya Morocco, Abderazzak Khairi watakutana na waandishi wa habari kesho (Aprili 19 mwaka huu) kuzungumzia mechi yao itakayofanyika Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkutano huo ambao pia utawahusisha manahodha wa timu hizo mbili utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Barabara ya Uhuru na Shaurimoyo.

Timu hizo zitakutana katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano itachezwa nchini Morocco wiki mbili baadaye.

JKT RUVU, YANGA KUUMANA JUMAPILI
Yanga ambayo inafukuzia kwa karibu taji la Ligi Kuu ya Vodacom itapambana na JKT Ruvu katika mechi pekee ya ligi hiyo wikiendi hii itakayofanyika Jumapili (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya mechi hiyo, nyingine zitakazochezwa mwezi huu ni kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayofanyika Aprili 24 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Aprili 25 ni kati ya Ruvu Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nayo Coastal Union itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mechi itakayochezwa Aprili 27. Uwanja wa Taifa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Simba na Polisi Morogoro itakayofanyika Aprili 28.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Thursday, April 11, 2013

WALIMU WAPINGA MPANGO WA SERIKALI KUSHUSHA ALAMA ZA UFAULU

Kufuatia kauli ya Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Philipo Mulugo kusema kuwa serikali inakusudia kushusha alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuelekea kidato cha tano na cha sita, wananchi pamoja na baadhi ya walimu ambao hawakupenda kutajwa majina yao wamesema kuwa njia hiyo sio suluhisho la kuinua elimu nchini bali kuzidi kudidimiza.

Wakiongea mjini hapa Kigoma, wamesema kushusha huko alama kutakuwa kunamfurahisha mwanafunzi na wazazi wake katika makaratasi huku mwanafunzi huyo kichwani hakiwa hajaelimika vya kutosha.

Wameongeza na kusema serikali inatakiwa kuhakikisha inatafutia ufumbuzi wa kudumu matatizo ya elimu yaliyopo kama nyezo za kufundishia, kuongeza idadi ya walimu sanjari na mishahara pamoja na ujenzi wa nyumba zao.

Akiongea katika mkutano na wamiliki wa shule za sekondari nchini uliofanyika mjini Mbeya, Naibu waziri Mulugo amesema kuwa mpango huo wa kushusha alama ya ufaulu kwa kidato cha nne utasaidia kutoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kupata nafasi ya kusoma kidato cha tano na cha sita.

KOCHA RHINO APIGWA FAINI, AFUNGIWA MECHI SITA


KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.

Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure uwanjani.

Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.

Nao wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.

Klabu ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.

Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.

Tuesday, April 9, 2013

MLIMANI TV KATIKA

Kigoma yakabiliwa na uhaba wa walimu wa sayansi.

Imeelezwa kuwa mkoa wa Kigoma unakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa somo la sayansi hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.

kauli hiyo imetolewa na Afisa elimu msaidizi wa Kigoma bwana Venance Babukege wakati akizungumzia maendeleo ya elimu ya mkoa huo.

Bwana Babukege amesema idadi wa walimu wa masomo ya sanaa inaridhisha huku upande wa sayansi hali ni mbaya zaidi hivyo kusababisha wanafunzi wengi wasichague michepuo ya masomo hayo huku wale waliochagua nao wakipata matokeo ambayo hayaridhishi.

kwa upande wa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi, babukege amesema wamekuwa wakiomba uhamisho pindi wanapopangiwa kigoma kutokana na kukosekanika nyenzo za kufundishia kwa vitendo.

katika mipango ya kujipanga kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka hususa kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka huu, Babukege amesema kuwa hivi sasa kitengo chake kinatembelea katika shule zote za sekondari za mkoa kuzungumza na walimu ili kupata njia ambazo zitasaidia kuinua kiwango cha ufaulu.

Anuary- Kigoma.

Monday, April 8, 2013

TABORA NA MASOMO YA JIONI KWA KIDATO CHA NNE

Mkoa wa Tabora umeamua kutoa nafasi za masomo ya jioni kwa wanafunzi waliofeli kidato cha nne hivi karibuni ili kuwapa nafasi waweze kusawazisha makosa yao na hatimaye waendelee na masomo ya ngazi ya juu.
Afisa elimu wa mkoa huo Midamo Paul Makungu amesema kuwa ofisi yake imeshakubaliana na walimu wa shule za sekondari kuanzisha masomo hayo kwa wanafunzi watakaopenda.