Karibu katika blog yetu

Thursday, April 11, 2013

WALIMU WAPINGA MPANGO WA SERIKALI KUSHUSHA ALAMA ZA UFAULU

Kufuatia kauli ya Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Philipo Mulugo kusema kuwa serikali inakusudia kushusha alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuelekea kidato cha tano na cha sita, wananchi pamoja na baadhi ya walimu ambao hawakupenda kutajwa majina yao wamesema kuwa njia hiyo sio suluhisho la kuinua elimu nchini bali kuzidi kudidimiza.

Wakiongea mjini hapa Kigoma, wamesema kushusha huko alama kutakuwa kunamfurahisha mwanafunzi na wazazi wake katika makaratasi huku mwanafunzi huyo kichwani hakiwa hajaelimika vya kutosha.

Wameongeza na kusema serikali inatakiwa kuhakikisha inatafutia ufumbuzi wa kudumu matatizo ya elimu yaliyopo kama nyezo za kufundishia, kuongeza idadi ya walimu sanjari na mishahara pamoja na ujenzi wa nyumba zao.

Akiongea katika mkutano na wamiliki wa shule za sekondari nchini uliofanyika mjini Mbeya, Naibu waziri Mulugo amesema kuwa mpango huo wa kushusha alama ya ufaulu kwa kidato cha nne utasaidia kutoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kupata nafasi ya kusoma kidato cha tano na cha sita.

No comments:

Post a Comment