Karibu katika blog yetu

Wednesday, January 30, 2013

WAHISANI WAKUSANYA PESA ZA KUISAIDIA MALI




Mkutano wa Kimataifa uliowaleta pamoja Viongozi wa nchi za Afrika na Maofisa wa Kimataifa umefanikiwa kukusanya jumla ya dola milioni 600 kwa ajili kusaidia vita vinavyoendelea Kaskazini mwa Mali. Wafadhili mbalimbali wamechangia fedha kwa ajili ya kuendeleza vita iliyopewa jina Vita ya Kupambana na Ugaidi Kaskazini mwa Mali lengo likiwa ni kuyasambaratisha Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanatawala kwa miezi zaidi ya tisa.

Mkutano huo umefanyika nchini Ethiopia ambapo mataifa hayo yameahidi pia kuchangia kijeshi ili kufanikisha kukabiliana na vitendo vya kigaidi ambavyo vyanzo vyake vimekuwa vikitanjwa kuwa nchini Mali.

Japan imechangia dola milioni 120 huku Marekani ikitoa kitita cha dola milioni 96 kati ya dola milioni 600 ambazo zimeahidiwa kutoka kwa nchi ambazo zimehudhuria mkutano huo maalum wa kuchangisha fedha.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa UN, Umoja wa Ulaya EU na China ambao wote wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia operesheni hiyo ya kijeshi.

Rais wa Mali Dioncounda Traore ameishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa mchango ambao wameutoa kwa nchi hiyo katika na kuahidi watakuwa tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali.

Umoja wa Afrika AU umeahidi kutoa dola milioni 50 kusaidia operesheni hiyo ya kijeshi huko Kaskazini mwa Mali ambayo imekadiriwa kugharimu dola milioni 460 ili iweze kukamilika.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AU Nkosazana Dlamini-Zuma amesema wanafahamu kitovu cha mgogoro kwa hiyo ushirikiano ambao wanaupata kutoka Jumuiya ya Kimataifa utasaidia kupata jibu.
Mkutano huo wa kuchangisha fedha kusaidia vita nchini Mali umekuja kipindi hiki ambacho majeshi ya Ufaransa na Mali yakifanikiwa kuweka kwenye himaya yao Mji wa Timbuktu.

Balloteli arudi nyumbani




Mshambuliaji wa Italia Mario balloteli anatarajia kukamilisha taratibu zote za usajili za kujiunga na klabu ya Ac Milan ya Italia akitokea Manchester City ambako ameshindwa kuelewana na kocha wa klabu hiyo Roberto Mancini.

Kusajiliwa kwa Balloteli na Milan kumepokelewa kwa furaha na wachezaji wa zamani wa Milan Zlatan Ibrahimovic na Thiago Silva ambao wanaamini kuwa Balloteli atasaidia kuipa matokeo mazuri Rosseneri.

CAF WANAFURAHIA ZAMBIA KUTOLEWA- HERVE RENARD


Herve Renard




Baada ya kushuhudia timu yake ikiondolewa katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika mwaka huu, kocha mkuu wa Zambia Herve Renard amesema anajua fika kuwa shirikisho la soka Afrika Caf litakuwa na furaha baada ya waliokuwa mabingwa hao watetezi kuondolewa katika hatua ya makundi.

Renard amesema Caf walikuwa hawapendi kuona Zambia ikitetea ubingwa huo na hatimaye kushiriki kombe la mabara nchini Brazil kwa kuwa wanaamini kuwa Chipolopolo haichezi soka la kuvutia.

Kocha huyo raia wa Ufaransa ameongeza na kusema kuwa kutolewa kwao sio mwisho wa dunia hivyo wanatakiwa wajipange katika michuano ijayo.


Naye mlinda mlango wa Zambia Kennedy Mweene amewataka wachezaji wenzake wazidi kushikama katika kipindi hiki ili waweze kufanya vizuri katika michezo ya kuwania kufuzu kucheza kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Tuesday, January 29, 2013

KABANGE TWITE KUSUBIRI MSIMU UJAO YANGA


Mchezaji Alain Kabange Twite hataweza kuichezea Yanga msimu huu (2012/2013) baada ya klabu hiyo kuingiza nyaraka zenye upungufu wakati ikimuombea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System- TMS).

Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), baadhi ya nyaraka zenye upungufu katika maombi hayo ni mkataba kati ya Twite na Yanga, lakini vile vile makubaliano ya mkopo (Loan Agreement) kati ya Yanga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo ndiyo inayommiliki mchezaji huyo.

Ili mchezaji aweze kupata ITC kwa njia ya TMS, kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF kuna nyaraka kadhaa muhimu zinatakiwa kukamilika katika maombi hayo ili hati hiyo iweze kupatikana.

1+1= GESI YA MSIMBATI



Bila shaka ni watu wengi wameshalisikia jina la Ken Saro-Wiwa kutokana na umahiri wake wa kuandika riwaya lakini naamini pia kuna wengi ambao hawamfahamu kiundani mwanaharakati huyu ambaye alipigania haki za watu wa sehemu aliyokuwa anatokea ya Ogoni huko Nigeria ili ipate mgao sawa wa pato la mafuta ambayo yalikuwa yanapatikanika katika eneo hilo lakini pia alitaka kuhakikisha mazingira ya Ogoni yanalindwa dhidi ya uchafuzi uliokuwa unafanywa na kampuni ya Shell.

Nyota ya mwanaharakati huyu wala haikudumu kwani aliuwawa kwa kunyongwa kwa kile kilichosemekana kuwa alihusika katika mauaji ya machifu wa Ogoni.

Binafsi naamini kuwa serikali ya kijeshi ya wakati huo ya Nigeria na wale wote waliokuwa wanamampinga Saro-Wiwa walikuwa hawajamuelewa hata kidogo kile ambacho alikuwa anakizungumza na mbaya zaidi walikuwa wanafuata mkumbo wa watu ambao walikuwa na maslahi yao binafsi katika suala la mafuta wakati huo.

Yaliyotokea Ogoni na Ken Saro-Wiwa sio kwamba yanafanana na yale yanatokea Mtwara hivi sasa ila tu yanafafa  kimahesabu na hasa katika njia zake za kukokotoa japo hatuna uhakika na jibu litakuwa lipi.

Tumeshuhudia mwishoni kabisa mwaka jana wananchi wa Mtwara wakiandamana kupinga kutoka Mtwara mjini mpaka eneo la Msimbati ambalo ndipo gesi asilia inavunwa kupinga kusafirishwa kwa nishati hiyo mpaka jijini Dar es Salaam.


Baada ya maandamano hayo ambayo yalionesha na kuwaamsha wananchi wengi ndani na nje ya nchi msimamo wa watu wa Mtwara kwamba hawataki gesi ipelekwe kwingine ndipo sasa kauli mbalimbali zikaanza kutolewa na serikali ikionesha kusimamia msimamo wake wa kuendelea na mchakato wa kusafirisha gesi hiyo kuja Dar es Salaam.

Binafsi sikuridhishwa maelezo aliyoyatoa Waziri wa Nishati na Madini Professa Sospeter Muhongo ambaye naamini kabisa yeye ni msomi ndio maana anaitwa Professa.

Jambo ambalo sikuelewa na wala sielewi mpaka sasa ni kuhusiana na majibu aliyoyatoa Waziri kwa kuwapinga waziwazi tena bila kuuma maneno wananchi wa Mtwara, sasa Je alikuwa anawapinga kisomi, kisiasa ama ni kutokana na utashi wake mwenyewe kwani binafsi majibu aliyoyatoa naamini ndiyo yamekuwa chimbuko ama chanzo cha vurugu, kurushiana maneno hata mie mwenyewe kuandika hii makala na hata wewe msomaji kusoma makala hii.

Ki ukweli ni kwamba Mhe. Waziri alikosea, naamini kabisa yeye pamoja na wenzake ambao wanawapinga wakazi wa Mtwara hawajawaelewa kabisa nini wanachotaka.

Kama wanataka gesi ibaki Mtwara jibu ni rahisi tu, wanaweza wakaiacha ibakie huko huko na inawezekana isiwanufaishe chochote wakazi hao licha ya kwamba watakuwa wanaiona na kusikia ipo Msimbati.

kitu ambacho nasikiri ni kwamba, wananchi hawa wanataka kuona ni jinsi gani gesi hii itaweza kubadilisha maisha yao ya kila siku tena ya mwananchi wa hali ya chini kabisa. Hapa namaanisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii mfano afya, elimu, maji na mengineyo.

Tukumbuke kuwa wakazi hawa wanajua hali ikoje kwa watani zao waliopo Geita, Kahama, Mwadui na kwingineko kwenye madini hivyo wanaogopa kuishia mikono mitupu na kuendelea kuuza korosho ambazo nazo walitarajia kuinua maisha yao lakini ndo hivyo ndoto zao zikaenda na maji kama machozi ya samaki baharini.

Takwimu za elimu zinaonesha kuwa mikoa ya kusini mwa Tanzania hususa Mtwara na Lindi ndiyo ambayo imekuwa ikishika nafasi za mwisho katika matokeo mbalimbali ya elimu, kutokana na hilo wanafunzi wengi katika mikoa hiyo wamekuwa wakikosa nafasi za kufika mbali kielimu mfano Chuo Kikuu na hatimaye kujiajiri ama kuajiriwa ili kusaidia familia zao na jamii nzima inayowazunguka.

Matokeo hayo mabaya yanadhirisha pia kuwa pengine hakuna fungu zuri la fedha linaloelekezwa katika elimu katika mikoa hiyo hivyo kufanya hali kuwa mbaya na mbaya zaidi mikoa ya kusini kuonekana ni mikoa ya kuzalisha wafanyabiashara wadogo wadogo “machinga” na sio wasomi kama mikoa mingine.

Kama ningelikuwa mwanafunzi natakiwa nitoe jibu katika hesabu hii, naona kuwa serikali inatakiwa kuhakikisha inaboresha kwanza miundo mbinu ya mikoa ya kusini hususa mkoa wa Mtwara na Lindi, inaelekeza nguvu zaidi katika elimu kwa kuboresha majengo, vifaa mpaka kupatika kwa walimu wenye uwezo ambao watalipwa vizuri bila matatizo.

Kama hiyo haitoshi wakazi hawa wanataka kuhakikishiwa usalama wa maisha yao na hapa nazungumzia afya, hospitali ambazo zina wataalamu, vifaa na dawa za kutosha.

Pengine kwa kumalizia, ndugu zangu hawa wa Mtwara na wengine kusini wangependa nao kuona vijana wao wanapata ajira katika makampuni ama mashirika ambayo yanafunguliwa katika mikoa yao lakini sio tu kuona wageni hususa kutoka nje ya nchi ndio wanaofaidika zaidi.

Kwa jibu hili la hesabu naamini kabisa serikali itaweza kuwashawishi wakazi hao kusafirishwa kwa gesi kwenda kwingine ili angalau nao walau wapate neema ambayo wao wanaipata kwani Tanzania ni moja na itaendelea kuwa moja kwa amani na utulivu.

Anuary Mkama
0716-387577

Thursday, January 24, 2013

HAZARD AOMBA MSAHAMA KWA KUMPIGA TEKE MUOKOTA MIPIRA





 
Kiungo mchezeshaji wa klabu ya Chelsea ya England amewaomba radhi mashabiki wa soka kwa kitendo cha kumpiga teke kijana muokota mipira katika mchezo kati ya timu yake na Swansea wa kusaka tiketi cha kucheza fainali ya  kombe la ligi la nchi hiyo Capital One.

Hazard amesema kuwa nia yake haikuwa kumpiga teke kijana huyo bali alichokuwa anataka ni kupiga mpira lakini kwa bahati mbaya akampiga katika tumbo.

Kocha wa Chelsea Rafael benitez amesema kuwa suala la hazard ambaye alioneshwa kadi nyekundu baada ya tukio hilo litajadiliwa ndani ya klabu hivyo hawezi kulielezea kiundani.


Katika mchezo huo Chelsea ilikwenda suluhu na Swansea hivyo kuondolewa katika michuano hiyo na kuifanya Swansea sasa kucheza na Bradford katika mchezo wa fainali.

Anuary.                                    BBC