Karibu katika blog yetu

Monday, March 25, 2013

Dk. Ali Mohamed Shein akutana na Mhe. Xi

   
RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na kumueleza kuwa Zanzibar imefungua milango ya uwekezaji hivyo China inaweza kutumia fursa hiyo kwa kuekeza katika sekta mbali mbali za kimaendeleo.
 
Dk. Shein aliyasema hay leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa China Mhe. Xi Jinping huko katika ukumbi wa hoteli ya Serena Jijini Dar-es-Salaam.
 
Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Rais Xi  Jinping kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo na kusisitiza kuwa ziara yake hiyo itakuwa ni fursa ya pekee ya kuweza kuitangaza Zanzibar katika sekta ya uwekezaji ili Zanzibar nayo inufaike.
 
Alisema kuwa Zanzibar imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo inaikaribisha China  kuja kuekeza Zanzibar kwa lengo la kuzidi  kuimarisha uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili hizo.
 
Dk. Shein alitoa shukurani na pongezi kwa China kutokana na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta mbali mbali za kimaendeleo kwa kutambua mchango wake mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa China ni miongoni mwa nchi za mwanzo  zilizotambua Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
 
Alisema kuwa China imeweza kuunga mkono sekta mbali mbali za maendeleo na kusifu kazi nzuri inayofanywa na madaktari wa nchi hiyo ambao wanafanya kazi zao katika hospitali za Zanzibar pamoja na kusifu mchango wa nchi hiyo katika ujenzi wa hospitali ya Abdala Mzee kisiwani Pemba.
 
Dk. Shein alieleza kuwa China imeweza kusaida miradi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuipatia Zanzibar mikopo nafuu katika kuendeleza miradi ukiwemo mradi wa  maji safi na salama mnamo miaka ya 70, misaada katika sekta ya habari, nafasi za masomo, afya, miundombinu, ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume unaoendelea, mawasiliano na miradi mengineyo.

Stars yamuweka matatani Taoussi

Majaliwa ya kocha mkuu wa Morocco Rachid Taoussi kuendelea kuifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo yapo mashakani baada ya wadau wa soka wa Morocco kutaka kocha huyo ajiuzuru kutokana na kufungwa goli 3-1 na Tanzania katika mchezo wa kuwania kucheza kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Wadau hao wa soka nchini humo wamesema kuwa kocha huyo ameshindwa kuiletea timu yao mafanikio lakini wameponda pia kitendo chake cha kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi kilichocheza katika michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika na kile kilichopata kipigo cha aibu kutoka kwa Tanzania.

Morocco sasa inahitaji miujiza ili isonge mbele katika hatua nyingine ya kuwania nafasi ya kucheza fainali zijazo za dunia nchini Brazil.