Karibu katika blog yetu

Tuesday, January 29, 2013

1+1= GESI YA MSIMBATI



Bila shaka ni watu wengi wameshalisikia jina la Ken Saro-Wiwa kutokana na umahiri wake wa kuandika riwaya lakini naamini pia kuna wengi ambao hawamfahamu kiundani mwanaharakati huyu ambaye alipigania haki za watu wa sehemu aliyokuwa anatokea ya Ogoni huko Nigeria ili ipate mgao sawa wa pato la mafuta ambayo yalikuwa yanapatikanika katika eneo hilo lakini pia alitaka kuhakikisha mazingira ya Ogoni yanalindwa dhidi ya uchafuzi uliokuwa unafanywa na kampuni ya Shell.

Nyota ya mwanaharakati huyu wala haikudumu kwani aliuwawa kwa kunyongwa kwa kile kilichosemekana kuwa alihusika katika mauaji ya machifu wa Ogoni.

Binafsi naamini kuwa serikali ya kijeshi ya wakati huo ya Nigeria na wale wote waliokuwa wanamampinga Saro-Wiwa walikuwa hawajamuelewa hata kidogo kile ambacho alikuwa anakizungumza na mbaya zaidi walikuwa wanafuata mkumbo wa watu ambao walikuwa na maslahi yao binafsi katika suala la mafuta wakati huo.

Yaliyotokea Ogoni na Ken Saro-Wiwa sio kwamba yanafanana na yale yanatokea Mtwara hivi sasa ila tu yanafafa  kimahesabu na hasa katika njia zake za kukokotoa japo hatuna uhakika na jibu litakuwa lipi.

Tumeshuhudia mwishoni kabisa mwaka jana wananchi wa Mtwara wakiandamana kupinga kutoka Mtwara mjini mpaka eneo la Msimbati ambalo ndipo gesi asilia inavunwa kupinga kusafirishwa kwa nishati hiyo mpaka jijini Dar es Salaam.


Baada ya maandamano hayo ambayo yalionesha na kuwaamsha wananchi wengi ndani na nje ya nchi msimamo wa watu wa Mtwara kwamba hawataki gesi ipelekwe kwingine ndipo sasa kauli mbalimbali zikaanza kutolewa na serikali ikionesha kusimamia msimamo wake wa kuendelea na mchakato wa kusafirisha gesi hiyo kuja Dar es Salaam.

Binafsi sikuridhishwa maelezo aliyoyatoa Waziri wa Nishati na Madini Professa Sospeter Muhongo ambaye naamini kabisa yeye ni msomi ndio maana anaitwa Professa.

Jambo ambalo sikuelewa na wala sielewi mpaka sasa ni kuhusiana na majibu aliyoyatoa Waziri kwa kuwapinga waziwazi tena bila kuuma maneno wananchi wa Mtwara, sasa Je alikuwa anawapinga kisomi, kisiasa ama ni kutokana na utashi wake mwenyewe kwani binafsi majibu aliyoyatoa naamini ndiyo yamekuwa chimbuko ama chanzo cha vurugu, kurushiana maneno hata mie mwenyewe kuandika hii makala na hata wewe msomaji kusoma makala hii.

Ki ukweli ni kwamba Mhe. Waziri alikosea, naamini kabisa yeye pamoja na wenzake ambao wanawapinga wakazi wa Mtwara hawajawaelewa kabisa nini wanachotaka.

Kama wanataka gesi ibaki Mtwara jibu ni rahisi tu, wanaweza wakaiacha ibakie huko huko na inawezekana isiwanufaishe chochote wakazi hao licha ya kwamba watakuwa wanaiona na kusikia ipo Msimbati.

kitu ambacho nasikiri ni kwamba, wananchi hawa wanataka kuona ni jinsi gani gesi hii itaweza kubadilisha maisha yao ya kila siku tena ya mwananchi wa hali ya chini kabisa. Hapa namaanisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii mfano afya, elimu, maji na mengineyo.

Tukumbuke kuwa wakazi hawa wanajua hali ikoje kwa watani zao waliopo Geita, Kahama, Mwadui na kwingineko kwenye madini hivyo wanaogopa kuishia mikono mitupu na kuendelea kuuza korosho ambazo nazo walitarajia kuinua maisha yao lakini ndo hivyo ndoto zao zikaenda na maji kama machozi ya samaki baharini.

Takwimu za elimu zinaonesha kuwa mikoa ya kusini mwa Tanzania hususa Mtwara na Lindi ndiyo ambayo imekuwa ikishika nafasi za mwisho katika matokeo mbalimbali ya elimu, kutokana na hilo wanafunzi wengi katika mikoa hiyo wamekuwa wakikosa nafasi za kufika mbali kielimu mfano Chuo Kikuu na hatimaye kujiajiri ama kuajiriwa ili kusaidia familia zao na jamii nzima inayowazunguka.

Matokeo hayo mabaya yanadhirisha pia kuwa pengine hakuna fungu zuri la fedha linaloelekezwa katika elimu katika mikoa hiyo hivyo kufanya hali kuwa mbaya na mbaya zaidi mikoa ya kusini kuonekana ni mikoa ya kuzalisha wafanyabiashara wadogo wadogo “machinga” na sio wasomi kama mikoa mingine.

Kama ningelikuwa mwanafunzi natakiwa nitoe jibu katika hesabu hii, naona kuwa serikali inatakiwa kuhakikisha inaboresha kwanza miundo mbinu ya mikoa ya kusini hususa mkoa wa Mtwara na Lindi, inaelekeza nguvu zaidi katika elimu kwa kuboresha majengo, vifaa mpaka kupatika kwa walimu wenye uwezo ambao watalipwa vizuri bila matatizo.

Kama hiyo haitoshi wakazi hawa wanataka kuhakikishiwa usalama wa maisha yao na hapa nazungumzia afya, hospitali ambazo zina wataalamu, vifaa na dawa za kutosha.

Pengine kwa kumalizia, ndugu zangu hawa wa Mtwara na wengine kusini wangependa nao kuona vijana wao wanapata ajira katika makampuni ama mashirika ambayo yanafunguliwa katika mikoa yao lakini sio tu kuona wageni hususa kutoka nje ya nchi ndio wanaofaidika zaidi.

Kwa jibu hili la hesabu naamini kabisa serikali itaweza kuwashawishi wakazi hao kusafirishwa kwa gesi kwenda kwingine ili angalau nao walau wapate neema ambayo wao wanaipata kwani Tanzania ni moja na itaendelea kuwa moja kwa amani na utulivu.

Anuary Mkama
0716-387577

No comments:

Post a Comment