Karibu katika blog yetu

Thursday, July 25, 2013

MPOTO ALIA NA BONGO FLAVOUR!




Mwanamuziki na mtunzi wa mashairi mahiri nchini Mrisho Mpoto amesema wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Flavour) ni wafanyabiashara zaidi hivyo wanashindwa kutetea na kuitambulisha jamii ama hadhira inayowazunguka.

Mpoto amesema hayo na Mlimani TV wakati wa kongamano la Muziki wa Afrika lililoanza hii leo
 (25/07/2013) idara ya sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Msanii huyo anayejulikana kwa jina la "Mjomba" amesema kuwa tofauti na nchi kama Senegal ambayo ina Youssou n'dour na Marekani, Michael Jackson, Tanzania mpaka sasa hakuna msanii ambaye anaweza akawa kitambulisho cha sanaa ya muziki nchini.


Katika hatua nyingine, Mpoto amesema vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto kubwa ya kuutangaza muziki wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Kongamano la Muziki wa Afrika linaloendeshwa na idara ya sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linaendelea na linatarajia kufikia kilele chake siku ya jumamosi kwa wahadhiri, nguli mbalimbali wa muziki kutoka nchi mbalimbali duniani kuwasilisha mada kuhusiana na muziki.

Maxmillian John Ngube, Hawa, Shumu, Emmanuel Kihwelu

KAMERA YETU

Mkulima katika kijiji cha Chiwerere mkoani Lindi akipiga piga mahindi baada ya kuvuna

Binti akiweka mahindi sehemu nzuri baada ya kuyavuna katika kijiji cha Chiwerere Lindi

Daladala kutoka kijiji cha Kijiweni mpaka Lindi

Mvuvi katika kijiji cha Kijiweni, Lindi

Kijiji cha Tchezema kilichopo Mvomero mkoano Morogoro

Sunday, July 14, 2013

TBS: HATUWEZI KUBAINI SIMU FEKI

Shirika la viwango nchini TBS limesema kuwa kwa sasa halina teknolojia inayowawezesha wataalamu wake kubaini simu zisizo na viwango ama feki.

Afisa uhusiano wa TBS, Bi Roida Andusanile akiongea na Mlimani TV amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho shirika lake linajipanga kuhakikisha inapata teknolojia hiyo ili kudhibiti uingizwaji wa simu hizo ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika maeoneo mengi nchini hususa katika jiji la Dar es Salaam.

Anuary Mkama.

Sunday, June 16, 2013

Sabri Lamouchi aikubali Stars!


Thomas Ulimwengu



Nadir Haroub
Sabri Lamouchi


Juma Kaseja akijitahidi kuokoa mpira wa tuta uliopigwa na Yahya Toure


Thomas Ulimwengu



Juma Kaseja

Kim Poulsen akimlalamikia kamisaa kuhusiana na penalty

Kim Poulsen akiwalalamikia waaamuzi baada ya mapumziko
Licha ya timu yake kuibuka na ushindi mnono dhidi ya Tanzania, Taifa Stars, kocha mkuu wa Ivory Coast Sabri Lamouchi amesifu kiwango cha kilichooneshwa na Stars.
kocha huyo kijana amesema kuwa amefurahishwa zaidi na uwezo wa washambuliaji wa Stars ambao walikuwa wanaliandama lango la timu yake kila mara.

Nao wachezaji wa Stars, Juma Kaseja, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Nadir Haroub wameitaka serikali na TFF kuendelea kuipa maandalizi mazuri timu ya taifa kwa mashindano mengine yanayokuja.
                                        
Mbwana Samatta

Akiongea zaidi Mbwana Samatta anayecheza katika klabu ya TP Mazembe ya DRC amesema kuwa nafasi anayocheza kwa sasa kama winga wa pembeni imekuwa ngumu kwake kutokana na kulazimika kurudi nyuma kusaidia safu ya ulinzi tofauti na anapokuwa katika klabu ya TP Mazembe, lakini amesema anafurahia kucheza kwani ni nafasi aliyokuwa anacheza awali lakini pia Kim Poulsen ndiyo nafasi anayopenda zaidi kumuona akicheza.


kutokana na matokeo hayo sasa, Ivory Coast imeungana na Ethiopia, Misri na Tunisia kutinga katika hatua ya mtoano ya kutafuta wawakilishi watano pekee ambao wataliwakilisha bara hili katika fainali za dunia za mwaka 2014 nchini Brazil.

Thursday, May 30, 2013

KUTOKA SAVE THE CHILDREN






Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara hatari kwa mtoto anayezaliwa- Taarifa ya Shirika la Save the Children kuhusu Hali ya Wazazi Ulimwenguni - 2013

Save the Children imezindua taarifa yake ya Hali ya Wazazi Ulimwenguni leo, 7 Mei, 2013 ikiwa na faharasa ya hatari ya kuzaliwa (Birthday Risk Index) ikionesha kuwa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara zinabaki kuwa ukanda hatari kwa mtoto anayezaliwa.

Katika taarifa hiyo,Tanzania iko katika nafasi ya 10 miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa ulimwenguni. Kiafrika Tanzania ni nchi ya tatu kwa vifo  vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa baada ya Nigeria na DRC na kwa ukanda wa Afrika mashariki inaongoza. Vilevile, Tanzania inachangia asilimia 2% ya vifo vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa ulimwenguni, ambavyo huchangiwa zaidi na matatizo ya uzazi kabla ya muda wa kujifungua, ukosefu wa vifaa vya kujifungulia, na changamoto za kupata huduma kwa watoto wachanga, hususani kwa kina mama wanaoishi maeneo ya vijijini.

Tanzania imefanya mabadiliko makubwa ya kisera katika kupanua huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa. Pamoja na hilo, kwa mujibu wa taarifa hii, watoto 17,000 hufa katika siku zao za kwanza za kuzaliwa na pia watoto 48,000 hufa kila mwaka, hivyo kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya watoto wach


anga,” anasema Dk. Stephen Ayella, Mshauri wa Programu ya Afya wa Save the Children nchini Tanzania.


Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Mali, Sierra Leone, zina idadi kubwa zaidi ya vifo vya watoto wachanga ulimwenguni. Mathalani, kwa mujibu wa taarifa hiyo, nchini Somalia, mtoto anayezaliwa yuko katika hatari ya kufa mara 40 zaidi kuliko mtoto aliyezaliwa Luxembourg. Vifo vya watoto wachanga, hususani katika siku ya kwanza ya kuzaliwa ni ishara hali ya usalama wa wazazi kutokana na matatizo ya wakati wa kujifungua na hali ya mtoto mchanga ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa.


Ulimwenguni kote, watoto milioni moja hufa kila mwaka katika siku yao ya kwanza ya kuzaliwa ama kwa lugha nyingine watoto wawili hufa kila dakika, hivyo kuifanya siku ya kwanza kuwa siku ya hatari zaidi kwa maisha ya mtu karibu katika kila nchi ulimwenguni.

Takwimu za kitaifa zilizotolewa katika faharasa zinaangazia nchi nyingi ulimwenguni. Viashiria kama hatari za vifo wakati wa uzazi, vifo vya watoto chini ya miaka 5, idadi itarajiwayo ya miaka ya mahudhurio katika shule rasmi, pato la taifa na ushiriki wa wanawake katika uongozi wa serikali vimetumika katika kupanga nafasi. Kati ya nchi 176 ulimwenguni, Tanzania ni nchi ya 135, ikionesha kupanda kidogo ukilinganisha na mwaka jana ambapo ilishika nafasi ya 140.



Taarifa imebainisha mambo ya msingi yanayochangia katika idadi hiyo kubwa barani Afrika. Mambo hayo ni pamoja na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda, kama ilivyo katika mfano wa Malawi ambayo ina idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda na ambao wanazaliwa na uzito pungufu. Mambo mengine ni pamoja na afya duni za wazazi, uzazi katika umri mdogo, ambavyo vinawaweka wazazi katika hatari ya kupata matatizo wakati ya uzazi yakiwa ni pamoja na mtoto aliye tumboni kutokuwa katika kiwango kinachostahili na kuzaa kabla ya muda.


Mkurugenzi wa Save the Children wa Ukanda wa Afrika Magharibi na Kati, Natasha Quist, anasema: “Nchi za Afrika na jumuiya ya ulimwengu wanafanya juhudi za kumaliza vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika, hata hivyo kama tunataka kufikia lengo hili la kihistoria, kunahitajika juhudi za ziada kuelekezwa katika kunusuru maisha ya watoto katika siku na miezi yao ya kwanza ya kuzaliwa.”

Wataalam wa masuala ya watoto wachanga wanakiri kuwa maendeleo makubwa yangeweza kufanyika kwa kueneza mbinu rahisi, zenye tija na gharama ndogo na kubadilishana mifano bora katika bara hilo.

Kupitia miradi yake ya Kuokoa Maisha ya Watoto Wachanga (SNL) na MAISHA, Save the Children nchini  Tanzania imekuwa mstari wa mbele nchini katika kuanzisha na kufuatilia huduma za Malezi kwa Mtindo wa Kangaroo (KMC), mtindo ambao ni maalum kwa kutunza watoto njiti na wenye uzito pungufu. Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Save the Children imeanzisha vituo 27 vya Malezi ya Mtindo wa Kangaroo Tanzania bara na Visiwani. Pia imefundisha zaidi ya wauguzi na madaktari 973 pamoja na kuwaelekeza juu ya Mtindo wa Kangaroo wafanyakazi 1185 wa kada zingine za afya.

Save the Children inakadiria kuwa maisha ya watoto wachanga milioni moja yanaweza kuokolewa kila mwaka, kuhakikisha upatikanaji wa vitu vinne tu ambavyo gharama yake ni ndogo: sindano za Corticosteroid kwa kina mama walio katika uchungu wa kabla ya muda, ambazo ni muhimu katika kupunguza vifo vitokanavyo na matatizo ya kupumua kwa watoto wanaozaliwa; vifaa vya kuamsha watoto wanaoshindwa kupumua baada ya kuzaliwa; dawa ya kusafishia baada ya kondo kutoka ili kuzuia maambukizi yanayotokana na kondo la nyuma na madawa ya sindano za kuzuia matatizo ya  kuvimba na kifua kwa watoto.

Vilevile, katika taarifa hiyo, Save the Children inaendelea kuonesha uhusiano kati ya afya ya mama mjamzito na vifo vya watoto wachanga. Faharasa hiyo ya Hali ya Wazazi Ulimwenguni inapanga huduma ambazo kila nchi inazitoa kwa kina mama kulingana na viashiria vya afya ya mama mjamzito, watoto chini ya miaka mitano, kiwango cha elimu kwa kina mama, kipato na hali ya kisiasa. Finland inaongoza ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inashika mkia.


Save the Children inatoa wito ufuatao kwa viongozi ulimwenguni:

§  Kuwekeza katika mambo yenye gharama nafuu na ambayo yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga. Madawa yanayoweza kutibu ama kuzuia maambukizi madogo madogo ambayo yanaweza kusababisha vifo. Vilevile kuhimiza unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee na malezi ya Mtindo wa Kangaroo, mambo ambayo hayana gharama yoyote, lakini yanaweza kuokoa maisha ya maelfu ya watoto.Vilevile, wahudumu wa kina mama wanaojifungua wanapaswa kupewa mafunzo, msaada na vifaa vya kutosha ili waweze kutoa huduma kwa ufasaha.


§  Kuimarisha mifumo ya afya ili kina mama wengi zaidi waweze kufikiwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi. Kuwekeza zaidi katika wahudumu wanaopokea wagonjwa na wahudumu wa afya katika jamii ili kuweza kusaidia kuwafikia kina mama na watoto walio katika hatari zaidi.
.
§  Kupambana na viini vya vifo vya watoto wachanga, usawa wa kijinsia na utapiamlo. Kusaidia kina mama kuwa na nguvu na imara-kimwili, kifedha na kijamii kunasaidia kuwawezesha watoto wao pia kuwa na nguvu na kuweza kuishi na kukua.

Dk. Rachel Makunde, Meneja Programu ya Afya ya Mama Wajawazito na Watoto wa Save the Children nchini Tanzania anatoa wito kwa serikali kuelekeza nguvu zaidi katika mipango na bajeti kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto, ikiwa ni pamoja na kueneza huduma ya Malezi kwa Mtindo wa Kangaroo hadi hospitali za wilaya na katika vituo vya afya.

“Kuzaliwa kabla ya muda kunachangia vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 35, kwa hivyo afua zenye kulenga watoto njiti zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watoto,” anasema.

Tuesday, May 28, 2013

Kongo yagawika pendekezo la Rais Kikwete


Pendekezo la Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo izungumze na makundi ya waasi na nchi jirani kutatua mzozo wa mashariki ya nchi hiyo linaonekana kuwagawa Wakongo.
Kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, kuna mwangwi wa sauti za Wakongomani wakiupongeza msimamo wa Rais Kikwete kwamba kuweko na mtazamo wa ujumla katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa kanda ya Maziwa Makuu.
Mwandishi wetu wa Kinshasa anaripoti kwamba wakaazi wengi wa mji huo wanaamini kuwa pendekezo hilo la Rais Kikwete linaweza kusaidia amani ya kudumu.
Kwenye mkutano wa marais 11 wa Nchi za Maziwa Makuu kwa ajili ya Kongo uliotishwa kando ya mkutano wa Umoja wa Afrika, mjini AddisAbaba, Rais Kikwete alipendekeza kufanyike mazungumzo baina ya Kongo na kundi la waasi la M23, Rwanda na kundi la waasi la FDLR na Uganda na waasi wake wa ADF/Nalu kwa ajili ya amani ya kudumu ya kanda ya Maziwa Makuu.
Tanzania inachangia wanajeshi 1,280 kwenye kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo,
Umoja usio wa kawaida Kinshasa
Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Joseph Kabila wa DRC.Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Joseph Kabila wa DRC.
Pendekezo hili limezua kile mwandishi wetu wa Kinshasa anachokiita “tukio la nadra kabisa nchini Kongo“ kwa wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala kuwa na kauli moja kuhusu maswala muhimu ya kitaifa.
Rais Kikwete amefanikiwa kuwaelekeza wanasiasa wa Kongo kuchukuwa msimamo wa pamoja kuhusu juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwenye kanda ya Maziwa Makuu.
Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ni kwamba Rais Kikwete aliwambia maraisi wenzake pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Afrika, kwamba ni lazima kuweko na mtizamo wa ujumla kwa ajili ya kumalizisha machafuko ya miaka mingi kwenye kanda la Maziwa Makuu.
Kwa hiyo Rais Kikwete alipendekeza Kongo kuendesha mazungumzo na waasi wa M23, na vilevile kuitaka Rwanda kuzungumza na waasi wa FDLR na Uganda kufungua mazungumzo na waasi wake wa ADF/Nalu. Pendekezo hilo limepongezwa na upinzani na chama tawala nchini Kongo, akiwemo mbunge Justin Bitakwira, ambaye ni kiongozi wa wabunge wa upinzani wa UNC.
Naye Franklin Tshamala, msemaji wa muungano wa vyama tawala, amesema kwamba pendekezo hilo la Rais Kikwete ni hatua ya ujasiri ya kutaka kurekebisha mitizamo tofauti waliyonayo viongozi wa mataifa haya matatu.
Rwanda yakataa
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
Pendekezo hilo la Rais wa Tanzania lilipongezwa pia na serikali ya Kongo. Akiwa mjini Addis Ababa, Waziri wa Mambo ya Nje ya Kongo, Raymond Tshibanda, aliiambia Radio France Internationale kwamba msimamo huo unalingana na ombi la miaka mingi la serikali ya Kongo kwa majirani zake.
Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, aliyehojiwa na redio hiyo hiyo alisema matamshi hayo ya Rais Kikwete ni ya upotofu na nchi yake haiwezi kamwe kuzungumza na watu waliohusika na mauwaji ya halaiki.
Magazeti mengi ya siku ya Jumanne (tarehe 28 Mei) yamezungumzia matamshi ya Rais Kikwete na maoni ya wananchi wa Kongo. Gazeti Lavenir limechapisha kichwa cha habari kwa wino mzito kikimuita Rais Kikwete ”Jjasiri wa kanda ya Maziwa Makuu.”
Kwenye ukarasa wa mwanzo, gazeti la upinzani la Tempetes des Tropiques limeandika “Kikwete arusha bomu Addis Abeba”, likiyaelezea matamshi ya Rais Kikwete kuwa sawa na bomu alilowarushia marais wenzake ambao kwa muda mrefu wameonyesha unafiki katika kumaliza machafuko ya Maziwa Makuu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Goma hawataki mazungumzo na M23
Wakimbizi wa ndani mashariki ya Kongo.Wakimbizi wa ndani mashariki ya Kongo.
Lakini hali ikiwa hivyo mjini Kinshasa, kwenye eneo la mashariki ya Kongo, ambako ndiko hasa kwenye mgogoro kati ya serikali na waasi wa M23, maoni ni tafauti.
Mwandishi wetu wa Goma, John Kanyunyu, anaripoti kwamba mashirika ya kiraia ya huko yamekataa mazungumzo baina ya serikali ya DRC na wajumbe wa M23.

Makamu mwenyekiti wa mashirika ya hayo kiraia katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ambaye pia ni msemaji wa mashirika hayo, Omar Kavota, amesema “hakuna tena la kuzungumza, kwani tayari mkataba wa M23 baina ya chama cha zamani cha uasi CNDP umeshajadiliwa.”

Kauli hiyo ya mashirika ya kiraia inakuja baada ya pendekezo la Rais Kikwete mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na marais wa kanda ya Maziwa Makuu kuiomba serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo baina yake na waasi wa M23.
Aidha kauli hiyo ya mashirika ya kiraia ya kuitaka serikali kutozungumza na wajumbe wa M23, inachochewa pia na utendaji kazi wa wanajeshi wa serikali katika uwanja wa mapigano.

Katika vita baina ya jeshi la serikali, FARDC, na waasi wa M23, jeshi hilo la serikali linatajwa kuwa, lilifaulu kwa mara ya kwanza kabisa, kuwazuia waasi wa M23 kuuteka upya mji wa Goma.

Kavota anasema ni bora zaidi kuwapatia nafasi ya kufanya kazi zao wanajeshi wa kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kinachowajumuisha wanajeshi kutoka Tanzania, Malawi na Afrika ya Kusini.
Katika kuwapongeza wanajeshi wa serikali kwa kazi waliyoifanya wakati wa mapigano ya wiki iliyopita, mashirika ya wanawake kutoka asasi za kiraia na vyama vya kisiasa, wametoa mchango wa pesa wa kile walichokiita “kuwanunulia wanajeshi wa serikali maji ya kunywa.”
Ripoti hii imetayarishwa na Saleh Mwanamilongo, Kinshasa, na John Kanyunyu, Goma
Mhariri: Mohammed Khelef

Friday, April 19, 2013

KUTOKA TFF


MECHI YA MGAMBO, YANGA YAINGIZA MIL 24/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mgambo Shooting na Yanga iliyochezwa jana (Aprili 17 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga imeingiza sh. 24,865,000 kutokana na watazamaji 4,386.

Viingilio katika mechi hiyo namba 162 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 vilikuwa sh. 10,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 5,547,337.50 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,792,966.10.

Asilimia 15 ya uwanja sh. 2,820,680.08, msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 90,000, waamuzi sh. 270,000, maandalizi ya uwanja sh. 100,000 na tiketi sh. 1,587,500.

Mgawo mwingine ni gharama za mechi sh. 1,692,408.05, Kamati ya Ligi sh. 1,692,408.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 846,204.05 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) sh. 658,158.69.

MAKOCHA AZAM, FAR RABAT KUTETA
Makocha wa timu za Azam, Stewart John Hall na AS FAR Rabat ya Morocco, Abderazzak Khairi watakutana na waandishi wa habari kesho (Aprili 19 mwaka huu) kuzungumzia mechi yao itakayofanyika Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkutano huo ambao pia utawahusisha manahodha wa timu hizo mbili utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Barabara ya Uhuru na Shaurimoyo.

Timu hizo zitakutana katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano itachezwa nchini Morocco wiki mbili baadaye.

JKT RUVU, YANGA KUUMANA JUMAPILI
Yanga ambayo inafukuzia kwa karibu taji la Ligi Kuu ya Vodacom itapambana na JKT Ruvu katika mechi pekee ya ligi hiyo wikiendi hii itakayofanyika Jumapili (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya mechi hiyo, nyingine zitakazochezwa mwezi huu ni kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayofanyika Aprili 24 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Aprili 25 ni kati ya Ruvu Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nayo Coastal Union itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mechi itakayochezwa Aprili 27. Uwanja wa Taifa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Simba na Polisi Morogoro itakayofanyika Aprili 28.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Thursday, April 11, 2013

WALIMU WAPINGA MPANGO WA SERIKALI KUSHUSHA ALAMA ZA UFAULU

Kufuatia kauli ya Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Philipo Mulugo kusema kuwa serikali inakusudia kushusha alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuelekea kidato cha tano na cha sita, wananchi pamoja na baadhi ya walimu ambao hawakupenda kutajwa majina yao wamesema kuwa njia hiyo sio suluhisho la kuinua elimu nchini bali kuzidi kudidimiza.

Wakiongea mjini hapa Kigoma, wamesema kushusha huko alama kutakuwa kunamfurahisha mwanafunzi na wazazi wake katika makaratasi huku mwanafunzi huyo kichwani hakiwa hajaelimika vya kutosha.

Wameongeza na kusema serikali inatakiwa kuhakikisha inatafutia ufumbuzi wa kudumu matatizo ya elimu yaliyopo kama nyezo za kufundishia, kuongeza idadi ya walimu sanjari na mishahara pamoja na ujenzi wa nyumba zao.

Akiongea katika mkutano na wamiliki wa shule za sekondari nchini uliofanyika mjini Mbeya, Naibu waziri Mulugo amesema kuwa mpango huo wa kushusha alama ya ufaulu kwa kidato cha nne utasaidia kutoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kupata nafasi ya kusoma kidato cha tano na cha sita.

KOCHA RHINO APIGWA FAINI, AFUNGIWA MECHI SITA


KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.

Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure uwanjani.

Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.

Nao wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.

Klabu ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.

Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.