Karibu katika blog yetu

Thursday, January 17, 2013

BAFANA BAFANA mhhhh!


Fainali zangu za kwanza za kombe la mataifa ya afrika kuangalia kikamilifu kuanzia mchezo wa kwanza mpaka wa mwisho zilikuwa ni za mwaka 1996 ambazo ziliandaliwa na Afrika Kusini ambao ndio tena wenyeji wa michuano ya mwaka huu.

Binafsi kabla ya kuanza kwa michuano hiyo sikuwa nawapa nafasi wenyeji wa michuano hiyo bafana bafana kutokana na kutokuwa na wachezaji wanaofahamika katika medani ya soka duniani ukilinganisha na Ghana iliyokuwa na Abeid Pele na Anthony Yeboah huku Zambia ikiwa na Kalusha Bwalya na Tunisia ikiwa imesheheni nyota waliokuwa wanacheza katika ligi ya Ufaransa.

Kadri fainali hizo zilivyokuwa zinaendelea ndipo nilipogundua ukali wa Bafana Bafana iliyokuwa na nyota wasio na majina makubwa kama Philipe Masinga, Mark William, Doctor Khumalo na John Shoes Moshoeu kiungo nyota ambaye mashabiki wengi walikuwa wanadhani ana sumaku mguuni.

Mwisho wa fainali hizo Afrika Kusini ikatwaa kombe hilo kwa kuilaza Tunisia goli mbili kwa bila, Mark Williams akitoka benchi na kufunga goli la pili lililomuhakikishia Mzee Madiba ndoto yake ya kuona raia wa Afrika Kusini wakisherehekea mafanikio ya nchi yao baada ya muda mrefu wa uhasama.

Miaka 17 imepita sasa toka mafanikio hayo makubwa zaidi, binafsi naamini inabidi uwe na moyo wa kutu kuweka shilling yako kwa Afrika Kusini kuwa watatwaa kikombe cha mwaka huu.

Sababu kubwa ni kuporomoka kwa soka la nchi hiyo, kukua kwa ligi ya Afrika Kusini kumetoa mwanya kwa klabu kusajili wachezaji wengi wa kigeni kutoka sehemu mbalimbali ili kutoa changamoto zaidi kwa wachezaji wa ndani, falsafa hii ndio inaibua kirusi cha ugonjwa ilionao Bafana Bafana kwa sasa ambao unaendana sawasawa na England wanaojiita Simba watatu.

Afrika kusini imejikuta ikipokea wachezaji wengi wakigeni hivyo kushindwa kutoa nafasi za wachezaji wazawa kutamba zaidi wakati ule ule kasi ya wachezaji wake kwenda kucheza soka la kigeni nje ya nchi hususa katika nchi zilizoendelea ikiwa ndogo sana ukilinganisha na mataifa ya magharibi mwa Afrika, Nigeria, Ivory Coast na Ghana.

Hali hii inasababisha kuwepo na nafasi finyu ya kuwapata wachezaji nyota ambao wanaweza wakaiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa hali aliyokutana kocha wa Afrika Kusini Gordon Igesund ambaye inambidi awe jeuri kuwaaminisha wapenzi wenye uzalendo wa hali ya juu kwa timu yao kuwa watatwaa ubingwa mwaka huu.

Nimalizie kwa kusema kuwa endapo Afrika Kusini itatwaa ubingwa mwaka huu basi nitaamini kweli kuna bahati katika mchezo wa soka na endapo pia Ivory Coast haitochukua kombe mwaka huu basi nitaamini mchezo wa mpira wa miguu sio wa haki ama haupo fair!

No comments:

Post a Comment