Karibu katika blog yetu

Thursday, May 30, 2013

KUTOKA SAVE THE CHILDREN






Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara hatari kwa mtoto anayezaliwa- Taarifa ya Shirika la Save the Children kuhusu Hali ya Wazazi Ulimwenguni - 2013

Save the Children imezindua taarifa yake ya Hali ya Wazazi Ulimwenguni leo, 7 Mei, 2013 ikiwa na faharasa ya hatari ya kuzaliwa (Birthday Risk Index) ikionesha kuwa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara zinabaki kuwa ukanda hatari kwa mtoto anayezaliwa.

Katika taarifa hiyo,Tanzania iko katika nafasi ya 10 miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa ulimwenguni. Kiafrika Tanzania ni nchi ya tatu kwa vifo  vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa baada ya Nigeria na DRC na kwa ukanda wa Afrika mashariki inaongoza. Vilevile, Tanzania inachangia asilimia 2% ya vifo vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa ulimwenguni, ambavyo huchangiwa zaidi na matatizo ya uzazi kabla ya muda wa kujifungua, ukosefu wa vifaa vya kujifungulia, na changamoto za kupata huduma kwa watoto wachanga, hususani kwa kina mama wanaoishi maeneo ya vijijini.

Tanzania imefanya mabadiliko makubwa ya kisera katika kupanua huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa. Pamoja na hilo, kwa mujibu wa taarifa hii, watoto 17,000 hufa katika siku zao za kwanza za kuzaliwa na pia watoto 48,000 hufa kila mwaka, hivyo kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya watoto wach


anga,” anasema Dk. Stephen Ayella, Mshauri wa Programu ya Afya wa Save the Children nchini Tanzania.


Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Mali, Sierra Leone, zina idadi kubwa zaidi ya vifo vya watoto wachanga ulimwenguni. Mathalani, kwa mujibu wa taarifa hiyo, nchini Somalia, mtoto anayezaliwa yuko katika hatari ya kufa mara 40 zaidi kuliko mtoto aliyezaliwa Luxembourg. Vifo vya watoto wachanga, hususani katika siku ya kwanza ya kuzaliwa ni ishara hali ya usalama wa wazazi kutokana na matatizo ya wakati wa kujifungua na hali ya mtoto mchanga ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa.


Ulimwenguni kote, watoto milioni moja hufa kila mwaka katika siku yao ya kwanza ya kuzaliwa ama kwa lugha nyingine watoto wawili hufa kila dakika, hivyo kuifanya siku ya kwanza kuwa siku ya hatari zaidi kwa maisha ya mtu karibu katika kila nchi ulimwenguni.

Takwimu za kitaifa zilizotolewa katika faharasa zinaangazia nchi nyingi ulimwenguni. Viashiria kama hatari za vifo wakati wa uzazi, vifo vya watoto chini ya miaka 5, idadi itarajiwayo ya miaka ya mahudhurio katika shule rasmi, pato la taifa na ushiriki wa wanawake katika uongozi wa serikali vimetumika katika kupanga nafasi. Kati ya nchi 176 ulimwenguni, Tanzania ni nchi ya 135, ikionesha kupanda kidogo ukilinganisha na mwaka jana ambapo ilishika nafasi ya 140.



Taarifa imebainisha mambo ya msingi yanayochangia katika idadi hiyo kubwa barani Afrika. Mambo hayo ni pamoja na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda, kama ilivyo katika mfano wa Malawi ambayo ina idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda na ambao wanazaliwa na uzito pungufu. Mambo mengine ni pamoja na afya duni za wazazi, uzazi katika umri mdogo, ambavyo vinawaweka wazazi katika hatari ya kupata matatizo wakati ya uzazi yakiwa ni pamoja na mtoto aliye tumboni kutokuwa katika kiwango kinachostahili na kuzaa kabla ya muda.


Mkurugenzi wa Save the Children wa Ukanda wa Afrika Magharibi na Kati, Natasha Quist, anasema: “Nchi za Afrika na jumuiya ya ulimwengu wanafanya juhudi za kumaliza vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika, hata hivyo kama tunataka kufikia lengo hili la kihistoria, kunahitajika juhudi za ziada kuelekezwa katika kunusuru maisha ya watoto katika siku na miezi yao ya kwanza ya kuzaliwa.”

Wataalam wa masuala ya watoto wachanga wanakiri kuwa maendeleo makubwa yangeweza kufanyika kwa kueneza mbinu rahisi, zenye tija na gharama ndogo na kubadilishana mifano bora katika bara hilo.

Kupitia miradi yake ya Kuokoa Maisha ya Watoto Wachanga (SNL) na MAISHA, Save the Children nchini  Tanzania imekuwa mstari wa mbele nchini katika kuanzisha na kufuatilia huduma za Malezi kwa Mtindo wa Kangaroo (KMC), mtindo ambao ni maalum kwa kutunza watoto njiti na wenye uzito pungufu. Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Save the Children imeanzisha vituo 27 vya Malezi ya Mtindo wa Kangaroo Tanzania bara na Visiwani. Pia imefundisha zaidi ya wauguzi na madaktari 973 pamoja na kuwaelekeza juu ya Mtindo wa Kangaroo wafanyakazi 1185 wa kada zingine za afya.

Save the Children inakadiria kuwa maisha ya watoto wachanga milioni moja yanaweza kuokolewa kila mwaka, kuhakikisha upatikanaji wa vitu vinne tu ambavyo gharama yake ni ndogo: sindano za Corticosteroid kwa kina mama walio katika uchungu wa kabla ya muda, ambazo ni muhimu katika kupunguza vifo vitokanavyo na matatizo ya kupumua kwa watoto wanaozaliwa; vifaa vya kuamsha watoto wanaoshindwa kupumua baada ya kuzaliwa; dawa ya kusafishia baada ya kondo kutoka ili kuzuia maambukizi yanayotokana na kondo la nyuma na madawa ya sindano za kuzuia matatizo ya  kuvimba na kifua kwa watoto.

Vilevile, katika taarifa hiyo, Save the Children inaendelea kuonesha uhusiano kati ya afya ya mama mjamzito na vifo vya watoto wachanga. Faharasa hiyo ya Hali ya Wazazi Ulimwenguni inapanga huduma ambazo kila nchi inazitoa kwa kina mama kulingana na viashiria vya afya ya mama mjamzito, watoto chini ya miaka mitano, kiwango cha elimu kwa kina mama, kipato na hali ya kisiasa. Finland inaongoza ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inashika mkia.


Save the Children inatoa wito ufuatao kwa viongozi ulimwenguni:

§  Kuwekeza katika mambo yenye gharama nafuu na ambayo yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga. Madawa yanayoweza kutibu ama kuzuia maambukizi madogo madogo ambayo yanaweza kusababisha vifo. Vilevile kuhimiza unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee na malezi ya Mtindo wa Kangaroo, mambo ambayo hayana gharama yoyote, lakini yanaweza kuokoa maisha ya maelfu ya watoto.Vilevile, wahudumu wa kina mama wanaojifungua wanapaswa kupewa mafunzo, msaada na vifaa vya kutosha ili waweze kutoa huduma kwa ufasaha.


§  Kuimarisha mifumo ya afya ili kina mama wengi zaidi waweze kufikiwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi. Kuwekeza zaidi katika wahudumu wanaopokea wagonjwa na wahudumu wa afya katika jamii ili kuweza kusaidia kuwafikia kina mama na watoto walio katika hatari zaidi.
.
§  Kupambana na viini vya vifo vya watoto wachanga, usawa wa kijinsia na utapiamlo. Kusaidia kina mama kuwa na nguvu na imara-kimwili, kifedha na kijamii kunasaidia kuwawezesha watoto wao pia kuwa na nguvu na kuweza kuishi na kukua.

Dk. Rachel Makunde, Meneja Programu ya Afya ya Mama Wajawazito na Watoto wa Save the Children nchini Tanzania anatoa wito kwa serikali kuelekeza nguvu zaidi katika mipango na bajeti kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto, ikiwa ni pamoja na kueneza huduma ya Malezi kwa Mtindo wa Kangaroo hadi hospitali za wilaya na katika vituo vya afya.

“Kuzaliwa kabla ya muda kunachangia vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 35, kwa hivyo afua zenye kulenga watoto njiti zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watoto,” anasema.

No comments:

Post a Comment