Karibu katika blog yetu

Friday, January 18, 2013

SIKU YA POSTA AFRIKA


Deus Mndeme- Poster Master




Tanzania imeungana na nchi nyingine za Afrika katika kuadhimisha siku ya posta barani Afrika

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es salaam,Posta Masta Mkuu Deus Mndeme amesema shirika la posta nchini linaadhimisha siku hiyo huku likijivunia ufanisi katika mipango yake mbalimbali

Ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupanuliwa na kuimarishwa kwa mtandao wa kutuma na kulipia fedha,kuimarishwa kwa usambazaji wa teknolojia mpya kwa ajili ya kuboresha huduma za intanet.

Amesema shirika hilo kwa hivi sasa limeanza kutumia mfumo wa kisasa wa intanet unaomwezesha mteja kufuatilia taarifa za barua au kifurushi  alichotuma

Posta masta huyo mkuu ameongeza kuwa shirika hilo linashirikiana na mamlak aya mawasiliano nchini TCRA katika  kubuni na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi

Katika hatua nyingine bwana Mndeme amesema hivi sasa shirika lake linataka kujiendesha kisasa zaidi ili kuzidi kuwashawishi vijana watumie huduma zao.

Thursday, January 17, 2013

BAFANA BAFANA mhhhh!


Fainali zangu za kwanza za kombe la mataifa ya afrika kuangalia kikamilifu kuanzia mchezo wa kwanza mpaka wa mwisho zilikuwa ni za mwaka 1996 ambazo ziliandaliwa na Afrika Kusini ambao ndio tena wenyeji wa michuano ya mwaka huu.

Binafsi kabla ya kuanza kwa michuano hiyo sikuwa nawapa nafasi wenyeji wa michuano hiyo bafana bafana kutokana na kutokuwa na wachezaji wanaofahamika katika medani ya soka duniani ukilinganisha na Ghana iliyokuwa na Abeid Pele na Anthony Yeboah huku Zambia ikiwa na Kalusha Bwalya na Tunisia ikiwa imesheheni nyota waliokuwa wanacheza katika ligi ya Ufaransa.

Kadri fainali hizo zilivyokuwa zinaendelea ndipo nilipogundua ukali wa Bafana Bafana iliyokuwa na nyota wasio na majina makubwa kama Philipe Masinga, Mark William, Doctor Khumalo na John Shoes Moshoeu kiungo nyota ambaye mashabiki wengi walikuwa wanadhani ana sumaku mguuni.

Mwisho wa fainali hizo Afrika Kusini ikatwaa kombe hilo kwa kuilaza Tunisia goli mbili kwa bila, Mark Williams akitoka benchi na kufunga goli la pili lililomuhakikishia Mzee Madiba ndoto yake ya kuona raia wa Afrika Kusini wakisherehekea mafanikio ya nchi yao baada ya muda mrefu wa uhasama.

Miaka 17 imepita sasa toka mafanikio hayo makubwa zaidi, binafsi naamini inabidi uwe na moyo wa kutu kuweka shilling yako kwa Afrika Kusini kuwa watatwaa kikombe cha mwaka huu.

Sababu kubwa ni kuporomoka kwa soka la nchi hiyo, kukua kwa ligi ya Afrika Kusini kumetoa mwanya kwa klabu kusajili wachezaji wengi wa kigeni kutoka sehemu mbalimbali ili kutoa changamoto zaidi kwa wachezaji wa ndani, falsafa hii ndio inaibua kirusi cha ugonjwa ilionao Bafana Bafana kwa sasa ambao unaendana sawasawa na England wanaojiita Simba watatu.

Afrika kusini imejikuta ikipokea wachezaji wengi wakigeni hivyo kushindwa kutoa nafasi za wachezaji wazawa kutamba zaidi wakati ule ule kasi ya wachezaji wake kwenda kucheza soka la kigeni nje ya nchi hususa katika nchi zilizoendelea ikiwa ndogo sana ukilinganisha na mataifa ya magharibi mwa Afrika, Nigeria, Ivory Coast na Ghana.

Hali hii inasababisha kuwepo na nafasi finyu ya kuwapata wachezaji nyota ambao wanaweza wakaiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa hali aliyokutana kocha wa Afrika Kusini Gordon Igesund ambaye inambidi awe jeuri kuwaaminisha wapenzi wenye uzalendo wa hali ya juu kwa timu yao kuwa watatwaa ubingwa mwaka huu.

Nimalizie kwa kusema kuwa endapo Afrika Kusini itatwaa ubingwa mwaka huu basi nitaamini kweli kuna bahati katika mchezo wa soka na endapo pia Ivory Coast haitochukua kombe mwaka huu basi nitaamini mchezo wa mpira wa miguu sio wa haki ama haupo fair!

Wednesday, January 16, 2013

MABWEPANDE: ELIMU BADO NI CHANGAMOTO

Picha kwa hisani.ya One Mocke Blog.

Upungufu wa walimu umeelezwa kuwa ni moja ya sababu zinazochangia matokeo yasiyoridhisha katika shule ya msingi Mabwepande iliyoko katika manispaa ya Kinondoni

Mwalimu mkuu wa shule hiyo  Davis Mkaruka amesema idadi ya walimu waliopo shuleni hapo haitoshelezi mahitaji halisi ya wanafunzi
Amesema shule hiyo ina jumla ya walimu 15 huku ikiwa na wanafunzi zaidi ya elfu moja

Mwalimu mkuu huyo amesema katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana wanafunzi 30 kati ya 94 ndio waliofaulu mtihani,matokeo ambayo amesema bado hayaridhishi

Ameiomba idara ya elimu katika manispaa ya Kinondoni kuongeza idadi ya walimu pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili walimu waweze kumudu mabadiliko ya mitaala

Monday, January 7, 2013

CUF YAWASILISHA MAONI YAKE KWA TUME YA KATIBA


Chama cha wananchi Tanzania CUF kimeshauri kwamba kuna umuhimu wa serikali TATU katika katiba mpya itakayoundwa ili kuondoa migongano na kero za Muungano.

Akiongea mara baada ya kutoa maoni yao kwa tume ya katiba,Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Haruna Lipumba amesema kuwa amesema muundo wa serikali tatu utalifaa taifa la Tanzania,amezitaja serikali hizo kuwa ni pamoja na serikali ya Tanganyika,Zanzibar na Muungano.

Profesa Lipumba amesema kuwa kumekuwepo na Malalamiko hasa kutoka upande wa Zanzibar kuwa serikali ya Tanganyika imemezwa nay a Muungano kutokana na muundo wa sasa.

Aidha katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amesema suala la rasilimali za nchi hiii zinatakiwa ziwekwe kikatiba ili kila mwananchi aweze kufaidi matunda ya Uhuru wa nchi hii.

Masuala mengine yaliyopendekezwa na chama hicho kwa tume ya katiba ni pamoja na suala la uteuzi wa viongozi, usawa wa kijinsia,maadili ya viongozi na kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi ili kutoa fursa sawa ya kidemokrasa katika  siasa.